Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo leo Machi 17, 2023 imekamilisha ziara yake ya jijini Dar es Salaam kwa kutembelea Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Moganzila ambapo imekagua Mradi wa kituo cha umahiri wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.

 Akiongea kwa niaba ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema Kamati imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kuahidi kuishauri Serikali kukamilisha awamu ya pili ya mradi ili kituo kikamilike.

 "Awamu ya pili ya mradi huu itahusisha ujenzi wa hospitali ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, inatakiwa nayo ikamilike ili chuo kinapotoa mafunzo wanafunzi wapate sehemu ya kufanyia mafunzo kwa vitendo," amefafanua Prof. Mkumbo.

 Kwa upande wake Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Wizara itashirikiana na Chuo kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge na kuahidi kuhakikisha awamu ya pili ya mradi inatekelezwa.

 Katika hatua nyingine Mkenda amesema Wizara haitavumilia tabia za wahadhiri na wakufunzi wanaodai rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa kike na kwamba yeyote atakayethibitika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.

 "Mwalimu akituhumiwa  kuwa unajihusisha na rushwa ya ngono hata kama hakuna ushahidi wa kutosha, tutamfuatilia kwa karibu bila yeye kujua hadi tufahamu ukweli kuhusu suala hilo," amesema Waziri Mkenda.

 Akitoa taarifa ya chuo Prof. Andrea Pembe, Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS amesema hatua waliyofikia sasa ni kuweka vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika kituo hicho cha umahiri wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kisha wataanzisha programu za mafunzo ili kituo kianze kutoa huduma.

 Amesema awamu ya kwanza ya mradi huu imegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 21.7 huku akiongeza kuwa chuo kwa sasa kina jumla ya programu 112 na wanafunzi 4,425.